Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Hujjatul-Islam wal-Muslimin, Ustadh Hamid Maliki, alizungumza kuhusu maudhui ya vita laini na mbinu za mashambulizi ya kiutamaduni kwa mtazamo wa Qur’an Tukufu, katika kipindi cha moja kwa moja cha televisheni kinachoitwa «Hayat-e Qur’ani» (Maisha ya Qur’ani), kinachorushwa kupitia Kituo cha Kimataifa cha Wilaya.
Vita laini; uadui unaojificha nyuma ya mwonekano mzuri na wa kuvutia
Naibu wa Mkurugenzi wa Hawza ya kielimu ya Qum alisema: Vita laini daima huingia katika uwanja wa mapambano vikiwa na mwonekano mzuri, wa kisanaa na wa kuvutia kwa namna ya udanganyifu, huku lengo lake likiwa ni kumfanya mwanadamu aghafilike na kumuepusha na njia ya haki.
Aliongeza kuwa, haipaswi kudhaniwa kwamba adui ni yule pekee anayeshika silaha; wakati mwingine adui hutumia njia ya urafiki na tabia za heshima ili kuathiri fikra na imani za mwanadamu, na hatua kwa hatua kumpotosha kutoka katika njia sahihi.
Umuhimu wa kutofautisha mwonekano wa udanganyifu na maudhui ya batili
Akisisitiza umuhimu wa kuwa na utambuzi na uelewa sahihi (Basira), alisema: Miongoni mwa sifa za vita laini ni kuwasilisha maudhui ya batili katika muundo mzuri na wenye kuvutia. Kwa sababu hiyo, mwanadamu anapaswa kuwa na uwezo wa kutofautisha kati ya mwonekano uliopambwa wa ujumbe na maudhui yake halisi.
Aliendelea kusema: Wakati mwingine pendekezo fulani huwasilishwa kwa lugha ya heshima, lakini njia inayolielekea haiendani na tunu za Mwenyezi Mungu. Katika mazingira kama hayo, mtu hapaswi kulikubali pendekezo hilo kwa sababu tu ya kuona haya kulikataa au kutaka kumridhisha anayelitoa.
Mtaalamu huyo wa masuala ya Qur’ani, akizungumzia nafasi ya sanaa na vyombo vya habari, alibainisha kuwa; mvuto wa nje unaweza kutumika katika kuwasilisha ujumbe wenye kujenga au maudhui yenye udanganyifu. Jambo muhimu ni kuzingatia maudhui ya ujumbe huo na athari zake katika imani na tabia za mwanadamu.
Mbinu nne za mashambulizi ya kiutamaduni kwa mtazamo wa Qur’ani
Hujjatul-Islam wal-Muslimin Maliki, alipokuwa akifafanua mbinu za mashambulizi ya kiutamaduni, alizitaja mbinu nne zifuatazo:
1. Kuifanya dini na Qur’ani ionekane kuwa haina umuhimu mkubwa
Wakati mwingine, kwa kuibua kauli kama vile: «Kuna ulazima gani wa kuswali?» au «Cha muhimu ni moyo kuwa safi», hujitokeza juhudi za kupunguza nafasi ya ibada katika maisha ya mwanadamu.
Swala na uhusiano na Mwenyezi Mungu havipaswi kuwekwa katika hali ya kupingana na shughuli za kiuchumi au majukumu ya kijamii. Badala yake, ibada inaweza kuwa msingi wa kupata utulivu wa kiroho na kuimarisha dhamiri katika utekelezaji wa majukumu ya kazi.
2. Kutoa madai yenye kuibua mashaka kuhusu imani za kidini
Kupitia kuibua maswali na shubha za aina hii: Ikiwa mafundisho ya dini ni ya kweli, kwa nini adhabu ya Mwenyezi Mungu haishuki mara moja? Hufanyika juhudi za kuziweka imani za kidini katika hali ya mashaka na kuzitia dosari.
3. Kuibua makelele na kuzuia sauti ya haki isisikike
Wakati mwingine, badala ya kutoa majibu kwa njia ya kimantiki, watu huibua makelele na vurugu kwa lengo la kuzuia sauti ya haki isisikike.
4. Kuitukuza na kueneza tamaduni za kijahilia
Baadhi ya tabia zisizofaa za zamani huwasilishwa kuwa ni mambo yenye thamani kwa sababu tu zinahusishwa na mababu na wazee waliotangulia. Hali hii ni pamoja na ukweli kwamba, kuwa jambo fulani limekuwepo kwa muda mrefu hakumaanishi kuwa ni jambo sahihi.
Kusisitiza umuhimu wa kurejea na kutafakari Aya za Qur’ani katika kukabiliana na vita laini
Naibu wa Mkurugenzi wa Hawza ya kielimu ya Qum, akirejelea Aya za 31 na 32 za Suratul-Anfal, alisema: Qur’ani Tukufu imeeleza mifano ya namna waliokataa haki walivyoitikia Aya za Mwenyezi Mungu, miongoni mwao ni kuziita Aya za Qur’ani kuwa ni «Asatirul-Awwalin» (hadithi na ngano za watu wa kale).
Alisisitiza kuwa Aya za Qur’ani zinaweza kutoa mwongozo katika kutambua mbinu zinazotumiwa kukabiliana na ujumbe wa haki, na kwamba kuifahamu elimu na maarifa ya Qur’ani humsaidia mwanadamu asidanganywe na mionekano ya nje yenye kuvutia.
Nafasi ya watu wanaoandamana na mwanadamu katika kujenga imani na mitazamo yake
Mwisho, alisisitiza umuhimu wa kuchagua kwa uangalifu mahusiano ya kijamii, akisema: Mwanadamu anapaswa kuwa makini na athari za watu wanaomzunguka katika fikra zake na mwelekeo wa maisha yake; kwani wakati mwingine kuandamana na mtu asiye sahihi kunaweza kumpeleka mwanadamu hatua kwa hatua mbali na tunu na misingi sahihi.
Mtaalamu huyo wa masuala ya Qur’ani alibainisha kuwa lengo la mafundisho ya Mwenyezi Mungu ni kuendeleza na kukuza vipawa na uwezo wa mwanadamu, pamoja na kumuongoza kuelekea katika maisha yaliyo bora na yenye kustahili.
Ikumbukwe kuwa: Kipindi cha moja kwa moja cha «Hayat-e Qur’ani» (Maisha ya Qur’ani) hurushwa kila siku ya Alhamisi kupitia Kituo cha Kimataifa cha Wilaya, huku Hujjatul-Islam wal-Muslimin Hamid Maliki akishiriki.
Maoni yako